Thursday, July 22, 2010

Slaa mgombea mpya URAIS 2010 CHADEMA

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano aliyepitishwa juzi na Kamati Kuu ya chama hicho, Dkt. Willibrod Slaa, atashinda katika uchaguzi mkuu ujao kwa kuwa hakuna wa kuweza kushindana naye. Akizungumza jana Makao Makuu ya chama hicho Kinondoni Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe alisema, "Dkt. Slaa anakwenda kushinda kiti hicho na si kushindwa kwa kuwa hakuna wa kushindana naye katika uchaguzi huo. "Dkt. Slaa anakwenda kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa ni mtu makini na ana upeo mkubwa wa kujua na kuchanganua mambo ni mzalendo na mwadilifu na mwenye uchungu na nchi yake hivyo ni mgombea mzuri anakwenda kushinda uchaguzi huo na kuchukua nchi." Wakati Bw. Mbowe akizungumza hayo, vyanzo vyetu vya habari vimesema kuwa pendekezo hilo la mgombea urais wa CHADEMA, limeibua mshituko kwa Chama cha Mapinduzi (CCM), ambapo imeripotiwa kuwa baadhi ya vigogo wameshtuka na kusema CCM kinahitaji kujipanga vizuri. Mtoa taarifa wetu alisema kuwa baada ya kupokea taarifa za kupendekezwa kwa Dkt. Slaa mapema jana, kigogo huyo alisikika akisema "kama ni Dkt. Slaa there is a need to go back to the drawboard" akimaanisha kuna umuhimu wa kujipanga upya. Bw. Mbowe alisema kuwa, Dkt. Slaa alipendekezwa baada ya kupokea, kujadili na kuzingatia taarifa ya utafiti kuhusu mgombea wa urais kupitia chama hicho kwa mujibu wa katiba ibara ya 7.7.1.6(a). Pia baada ya majadilino ya kina na kwa kuzingatia umuhimu wa kuziba ombwe la uongozi wa juu nchini. Alisema, hakuna wa kushindana naye katika uchaguzi huo hivyo aliwataka Watanzania kutopiga ramli za kukikatisha tamaa chama hicho kwa kuwa mipango iliyopangwa ni ya ushindi. Aliwatoa hofu wanachama wa chama hicho katika Jimbo la Karatu kuwa halitachukuliwa na chama kingine huku akisema Kamati Kuu ya CHADEMA ilimwona Dkt. Slaa, ndiye mgombea makini, mwenye upeo anayehitajika kuhuisha uzalendo na uadilifu nchini na kuzingatia kuwa urais kupitia chama hicho si jambo la binafsi bali la chama na nchi. Alisema Kamati Kuu ya chama hicho inawahakikisha Watanzania kuwa wananchi wa Karatu watapatiwa mbunge makini kupitia chama hicho atakayeziba kikamilifu pengo la Dkt. Slaa jimboni na bungeni. Bw. Mbowe alikanusha madai yaliyotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa Dkt. Slaa ametumwa na Kanisa Katoliki kugombea kiti hicho ambapo alisema, kamwe chama hicho hakifanyii kazi umbea kwa sababu hiyo haitafanya Dkt. Slaa kuacha kugombea nafasi hiyo. Alisema, CHADEMA haindeshwi kwa misingi ya dini bali inaheshimu imani zote za ukristo, uislamu na upagani, kwakuwa inaendeshwa kwa kufuata sheria na kanuni za chama hicho. Aliwataka, waandishi wa habari kuacha kuandika habari za kupikwa au kutumwa na wamiliki wa vyombo vya habari kwakuwa zinaweza kuibomoa nchi na kuhatarisha amani na utulivu uliopo. Akizungumuzia ushirikiano na vyama vingine Bw. Mbowe alisema, milango ya ushirikiano iko wazi kwa vyama makini kama Chama Cha Wananchi (CUF) na vingine lakini si vyote. "Hili lazima niseme na liwe wazi hatuko tayari kushirikiana na Chama kama TLP ambacho kiongozi wake alicheza ngoma na kuruka ruka katika mkutano CCM pale Dodoma au kumsifia kikwete," alisema Bw. Mbowe. Akitangaza kuhusu maazimio yaliyopitishwa na Kamati Kuu ya CHADEMA Bw. Mbowe alisema,kamati hiyo ilijiridhisha kuwa Dkt. Slaa ndiye mtu pekee anayefaa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alisema, wajumbe wa kamati hiyo kwa kauli moja walimuomba achukue fomu ya kugombea nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu ujao na alikubali, hivyo anasubiri kuchaguliwa kwa mgombea mwenza wake Agosti 12 pamoja na mgombea urais wa Zanzibar. Katika kamati hiyo mambo manne yalipitiwa ikiwa ni kupokea, kujadili na kupendekeza kwa Baraza Kuu rasimu ya ilani ya uchaguzi ya chama kwa ajili ya uchaguzi mkuu. Kupokea, kujadili na kupitisha taratibu zilizopendekezwa na Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) za kuwateuwa wabunge wa viti maalumu kupitia chama hicho. Pia alisema, kamati hiyo ilipokea, kujadili na kuzingatia maendeleo ya uchukuaji wa fomu za wagombea wa nafasi za udiwani uwakilishi na ubunge katika halmashauri na majimbo mbalimbali. Wakati huo huo watu mbalimbali wametoa maoni yao kuhusu Dkt. Slaa kupendekezwa kuwa mgombea urais na chama chake, ambapo baadhi ya wachambuzi wa mambo ya siasa wamepongeza na kusema kuwa hatua hiyo italeta changamoto kwa wagombea wa nafasi hiyo. Mbali na kuleta changamoto, pia wamesema Dkt. Slaa ana uwezo hivyo anafaa kusimama na kugombea nafasi hiyo kwa kuwa ni mtu makini, mwadilifu, msomi na mtetezi wa wanyonge na si mtu wa maneno matupu. Akizungumza na Majira kwa njia ya simu, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Bukoba Methodius Kilaini, alisema kuwa kwa upande wake kwa sasa hawezi kusema chochote zaidi ya kumtakia kila la heri katika mapambano ya kusaka nafasi hiyo. “Jamani nikisema kwa sasa si mtaniambia nafanya kampeni?...huo moto uwasheni huko huko lakini ninachoweza kusema kwa muda huu ni kumtakia heri,” alisema Askofu Kilaini. Naye Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Bi. Ananilea Nkya, alisema kuwa Dkt. Slaa anafaa kuwania nafasi hiyo kwa kuwa ni mtu makini katika kufanya kazi zake. “Dkt. Slaa ni mwanasiasa makini na mwenye sifa tele za uongozi katika kufanya kazi zake, ni mtetezi wa wanyonge, ni jasiri anayejitoa mhanga kutetea maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla,” alisema Bi. Nkya. Alisema kuwa ndani ya miaka mitano ambayo amekuwa Mbunge wa Jimbo la Karatu amekuwa mfano kwa wabunge wengine hasa kwa namna alivyowawakilisha wananchi wake na anavyoshughulikia matatizo jimboni na ya nchi. Bi. Nkya ambaye ni mshindi wa Tuzo ya Mwanamke Jasiri mwaka 2010, inayotolewa na Marekani, aliongeza kuwa uamuzi wake wa kuwania nafasi hiyo utatoa changamoto kwa wagombea wengine kwa kuwa Dkt. Slaa ni mtendaji halisi. “Taifa likipata mtu kama alivyo Slaa mambo yatakwenda vizuri sina hofu na utendaji wa kazi yake,” alisema. Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa CCM Bw. Pius Msekwa alisema kuwa uteuzi huo haukinyimi usingizi chama chake kwa kuwa hautampunguzia ushindi wa kishindo mgombea wao Rais Jakaya Kikwete. Akizungumza na Majira jana, Bw. Msekwa alisema kujitokeza kwa Dkt. Slaa ni matokeo kustawi kwa demokrasia nchini na kwamba wanaomba vyama vingine pia kutangaza wagombea wao. “Sisi kama wana CCM tunaona kujitokeza kwa Dkt. Slaa ni dalili ya kukolea kwa demokrasia nchini, mimi naona hili ni jambo jema sana kustawisha demokrasia nchini, tunawaomba na vyama vingine vyote vyenye usajili wa kudumu wasimamishe wagombea ili kukoleza zaidi demokrasia. Alipoulizwa taarifa kwamba CCM imepanga kuwa na Kikao maalum cha Kamati Kuu (CC) kuwejiweka sawa katika uchaguzi mkuu ujao alikanusha na kusisitiza kwamba ratiba ya CC ya kukaa Agost 13 ipo palepale na wala haijabadilika kama inavyodaiwa. Kuhusu ratiba ya kura za maoni inayoanza leo hadi Julai 31 alisema ni matarajio yao kwamba mchakato huo utafanyika vizuri na kuleta mapinduzi makubwa ya demokrasia ndani ya CCM. Imeandaliwa na Edmund Mihale, Sophia Kilumanga, Grace Michael, Tumaini Makene na John Daniel.

Chanzo Habari: www.majira.co.tz

No comments:

Post a Comment